Mambo Ya Ajabu Yaonekana Kwenye Kuaga Maiti 12 Za Ajali Iliyoua 20 Tanga


Ni msiba juu ya msiba. Yanakosekana maneno ya kutafsiri kilichotokea katika viwanja vya Hospitali ya Huruma, Wilaya ya Rombo ambako lilifanyika zoezi la uagaji miili ya watu waliokufa katika ajali kule mkoani Tanga, ndugu walikua wanaanguka na kuzimia uwanjani hapo wakati maiti za wapendwa wao zikiwa kwenye majeneza, Mwananchi imeripoti.


Ajali hiyo ilitokea Februari 4 usiku katika eneo la Magira Gereza, Kata ya Magira Gereza, Wilaya ya Korogwe, barabara ya Segera- Buiko mkoani Tanga. Na imesababisha vifo vya watu 21 mpaka sasa, huko mmoja kati ya hao- akiwa ni marehemu aliyekua akisafirishwa kwa mazishi kule Moshi.


Ndugu na majirani waliambatana viwanjani hapo kuaga miili ya ndugu zao wa ukoo mmoja, waliofariki ajalini wakiwa katika zoezi la kuusindikiza mwili wa Athanas Mrema aliyekua na miaka 59. Athanas alifariki Februari Mosi na mazishi yake yalipangwa kufanyika kule Moshi, ambapo ajali hiyo ilipatikana wakati wa safari ya kuusafirisha mwili wake.


Kwenye mazishi ambayo yamefanyika jana, ipo familia moja ambayo kwa bahati mbaya, iliathiriwa sana na ajali hiyo na inazika watu watano kwa wakati mmoja. Wote hawa ni wa familia moja. Wakati huo huo familia nyingine inazika wawili pamoja na wengine ambao wanazikwa mwili mmoja mmoja, maafa yalotokana na ajali hiyo mbaya iliyogusa karibu kila mtu nchini.


Awali ilitoka taarifa ya kuwa miili 16 ingeagwa katika viwanja hivyo. Lakini, ni miili 12 pekee ambayo iliagwa kwa ajili ya maziko ambayo yanafanyika katika familia iliyopoteza watu 14 kwenye ajali hiyo. Fahamu tu, kati ya vifo vyote 21, achana na habari za awali ziloripoti vifo 17- watu 14 kati yao ni ndugu wa familia moja.


Tayari- Athanas (Marehemu aliyekua anasafirishwa) kaishazikwa huko huko Rombo kama ilivyokua imepangwa.


Zoezi la kuiaga miili mingine 12, lilianza majira ya saa mbili asubuhi jana Februari 6. Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu aliongoza zoezi hilo kwa kushirikina na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa.


Kiongozi huyo alisema wilaya hiyo imeandaa magari 13 kwa ajili ya kubeba miili na yalikwenda kwa Eskoti ya Jeshi la polisi mpaka kwenye familia ambazo zimepoteza wapendwa wao.


Vile vile, baadhi ya miili ilizikwa katika Kitongoji cha Kirungu Mokala, Kata ya Kelamfua Mokala kule Keryo, Mengwe na Shimbi wilayani Rombo.

Comments